Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya nchini Somalia imeamuru kuzimwa kwa mitandao ya kijamii TikTok na Telegram ikisema imefanya hivyo kwa sababu za kiusalama pamoja na kupambana na ugaidi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Arab news hatua hiyo imekuja baada ya madai kuwa mitandao hiyo inatumiwa na magaidi katika kueneza propaganda.
Katika taarifa yake iliyotoka jana Jumapili Agosti 20, 2023, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, Jama Hassan Khalif, imesema ukiukaji wa mara kwa mara wa vikundi vya kigaidi vinavyotumia mitandao ya kijamii huathiri usalama na utulivu wa jamii.
Katika kutekeleza hilo Wizara imeagiza watoa huduma za mtandao hadi kufikia Agosti 24 wawe wameshatekeleza hilo.
"Katika jitihada za kutokomeza magaidi ambao wamemwaga damu ya watu wa Somalia, Waziri anaagiza makampuni yanayotoa huduma za mtandao kusitisha TikTok, Telegram na kampuni ya kamali ambayo magaidi na makundi yanahusika kueneza klipu za picha, na kupotosha jamii,” imeeleza taarifa hiyo.
Wizara hiyo imesema inafanya kazi kulinda maadili ya watu wa Somalia wakati wa kutumia zana za mawasiliano na mtandao ambazo zimeathiri mfumo wa maisha na zimeongeza mazoea mabaya.
Source: Mwananchi