YALIYOJIRI LEO AGOSTI 21, 2023 WAKATI WA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA (KKKT) YALIYOFANYIKA JIJINI ARUSHA

#Nimepewa heshima ya kuweka jiwe la msingi kwenye maabara ya sayansi ya Chuo cha Tumaini, nimeangalia vilivyopo ndani, mmefanya jambo kubwa sana. Hii ni katika hatua za kukua kwa kanisa hili la KKKT.


#Miaka 60 ya KKKT imekuwa na faida kwa waumini na Watanzania kwa ujumla, hii ndio sababu sote kwa pamoja tupo hapa kusheherekea siku hii.


#Mdau yeyote anayefanya kazi ya kumuhudumia mwananchi, anaisaidia Serikali katika kutekeleza wajibu wake na ndio maana miaka yote tumeendeleza ushirikiano na taasisi za dini na wadau wengine wote katika kuwahudumia Watanzania.


#Serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazojitokeza katika ushirikiano wetu chini ya Sera ya PPP ili kwa pamoja tuendelee kumuhudumia mwananchi ipasavyo.


#Serikali ya Awamu ya Sita imejidhatiti kuimarisha misingi ya utawala bora inayozingatia sheria, demokrasia na maadili yetu kama Watanzania, binafsi nimedhamiria hivyo na ndivyo ninavyowaelekeza wasaidizi wangu.


#Baada ya kuona adhabu tunazopata za mabadiliko ya tabianchi kutokana na kutotunza mazingira katika nchi yetu ambayo kwa asilimia kubwa inategemea kilimo, naomba wote tuwe rafiki wa mazingira.


#Nafarijika kuona viongozi wa dini wanasisitiza suala hili, natamani taasisi za dini kujiwekea mikakati mahsusi ya kupambana na uharibifu wa mazingira.


#Nawahakikishia kuwa, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa taifa hili, kuuza taifa hili wala kuharibu amani na usalama tuliojenga kwenye taifa hili.


#Serikali inawategemea sana viongozi wa kiroho katika kukuza, kusimamia na kuenzi maadili  ya watoto wetu ili waje kuwa vijana wazuri wa taifa la baadae, lazima tutunze mila na desturi zetu zile njema zilizotukuza kuwa hapa tulipo na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.


*Aliyosema Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Fredrick Shoo*

Uploading: 528175 of 528175 bytes uploaded.



#Uwepo wako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye tukio hili maalum la Maadhimisho ya Miaka 60 ya KKKT unadhihirisha jinsi ambavyo wewe mwenyewe na Serikali unayoiongoza inavyothamini mchango wa taasisi za dini katika jamii yetu.


#Tangu kuanzishwa kwa kanisa hili, tumefanya kazi sio tu ya kupeleka injili kwa watu bali tumetoa huduma za jamii, tumekuwa mstari wa mbele katika kutimiza wito katika kumuhudumia mwanadamu kiroho, kimwili na kiakili.


#Kanisa limejikita katika kutoa huduma za jamii ikiwemo huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi ngazi ya Hospitali ya Rufaa, elimu kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu, vyuo vya ufundi na elimu kwa watu wenye mahitaji maalum.


#Kanisa pia limejikita katika huduma ya utetezi, kupinga ukatili, kuwasaidia wale walioathirika kwa namna yoyote, ukatili wa kijinsia, dhidi ya wenye ulemavu wa ngozi na ukatili dhidi ya ukeketaji.


#Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Kanisa uliodumu kwa muda mrefu, ushirikiano huu umezingatia ustawi wa wananchi wa Tanzania pasipo ubaguzi.


#Ni maombi yangu kuwa asiwepo mtu mwenye kupotosha juu ya ushirikiano huu kwani ni historia ya kweli kuwa taasisi za dini zimechangia kikubwa sana kwa maendeleo ya nchi yetu kabla na baada ya Uhuru.


#Tunakushukuru kwa ukarimu wako wa kuona haja ya Watanzania wanaoteseka kwa magonjwa ya Saratani kwa kukubali kujenga banka kwa ajili ya kutibu Saratani ambapo Serikali inagharimia banka hilo kwa gharama ya shilingi bilioni 5. Mradi huo umefikia 70%.


#Nakupongeza kwa kazi kubwa unazofanya kwa ajili ya nchi yetu, kushika kwako nafasi ya Urais ni mpango wa Mungu kwako, naomba uendelee kufanya kazi yako ukijiamini na kwa ujasiri. Hakika tumeshuhudia miradi yote ikiendelezwa kwa kasi ya kuridhisha na kuibuliwa kwa miradi mipya.


#Umedumisha amani, upendo, mshikamano miongoni mwa Watanzania wote kwa kukuza Diplomasia ya Uchumi, kukuza uhuru wa kuongea, Demokrasia ya Vyama vya Siasa kupitia falsafa yako ya R nne, napongeza sana falsafa yako ya kujenga uchumi unaotegemea sekta binafsi ili kukuza ajira nchini.


#Naomba ieleweke kuwa Kanisa linaunga mkono uwekezaji, viongozi wa dini zote tulionana na wewe na kuwasilisha maoni yetu kuhusu uwejezaji katika bandari na ukaahidi kuwa maoni yetu utayapeleka kwa wataalam kwa ajili ya kufanyiwa kazi kwa uzito unaostahili na kwa maslahi mapana ya Taifa. Tuna imani na wewe, tunakuombea kwa Mungu ili hekima itumike katika kuleta muafaka wa jambo hili.


#Utunzaji wa mazingira ni jambo muhimu, naomba tulitilie mkazo jambo la utunzaji wa mazingira kwa ajili yetu na kwa vizazi vijavyo, natoa wito kwa viongozi wa dini na serikali kulifanyia kazi jambo hili. Nina imani Serikali yetu ina uwezo wa kuwekeza katika nishati itokanayo na jua na upepo, naomba tuingie huko.


#Umoja na mshikamano wa Tanzania ni muhimu kuliko mtu au kundi lolote, nawaomba viongozi wa dini na siasa kuacha kabisa kujaribu kuwagawa watu kwa misingi ya dini au itikadi za kisiasa na kwa misingi ya maslahi binafsi. Naiomba Serikali kukataa na kukemea kwa nguvu zote wale wote wanaoonesha dalili za kutugawa.


*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*

Post a Comment

Previous Post Next Post